Barcelona: Je Xavi ameiva kuwanoa wakali hao wa La liga ?

v

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Xavi ni mmoja wa wachezaji walioweka rekodi nyingi Barcelona
Iliyochapishwa

Gwiji la zamani la Barcelona, Xavi anatarajiwa kuthibitishwa kuwa Meneja mpya wa klabu hiyo, kumrithi Ronald Koeman aliyetimulia juma lililopita.

Tayari ujumbe maalumu ulishafika Qatari kuzungumza na klabu ya Al Sadd na Xavi anasema anataka kurejea nyumbani, akiamini kila kitu kitakuwa sawa kati ya Barcelona na klabu yake anayooinoa sasa ya Al Sadd.

"Nimekuwa nikizungumza na Barca kwa siku kadhaa sasa, kila kitu kitakuwa sawa. Klabu yangu inajua nataka nini na naamini watafikia muafaka," alisema kiungo huyo wa zamani wa Barca. Pamoja na uongozi wa Barca na mwenyewe Xavi kutaka kuanzisha safari mpya ya kuipaisha tena timu hiyo yako maswali manne muhimu ya kujiuliza.

1`: Xavi ameiva kuionoa Barcelona?

v

Chanzo cha picha, Getty Images

Hili ndilo swali kuu. Hakuna mwenye shaka na uwezo wa Xavi kama kiungo mwenye macho na pasi za uhakika, anayeweza kumiliki dimba atakavyo. Wakati akiichezea Barcelona na hata timu ya taifa ya Hispania, utafurahi kwa namna anavyomiliki dimba la kati. Lakini wengi wana wasiwasi na uwezo wake kama kocha.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 41, alibeba mikoba ya ukocha wa Al Sadd tangu mwaka 2019, akiwaongoza mabingwa hao wa Qatar kucheza michezo 89 akishinda 61 sawa 68.5% ni rekodi za kuvutia.

Katika msimu huu wa 2021/22, kikosi cha Xavi cha Al Sadd kinaendelea kusumbua kwenye ligi 'Qatar Stars League' kikishinda michezo yote saba, akitoka kuiongoza timu hiyo kushinda mataji matatu msimu uliopita. Licha ya kushinda mechi zake, Al Sadd inashinda kwa kishindo ikipachika mabao 29 mpaka sasa kwenye ligi. Pamoja na rekodi hizi nzuri, kurejea kwake Barcelona ni mtihani tosha kwake kuona kama amekomaa kuwafundisha wakali hao wa 'Laliga', kutokana na utofauti wa ligi hizi mbili, Qatar na Laliga.

'Ni mwanafunzi mzuri wa mchezo huu na amesoma vyema kwa undani kila nafasi inapaswa kuwajibikaje, mtu akiwa na mpira na asipokuwa na mpira', anasema Guillem Balague, mchambuzi wa BBC na kuongeza 'Jambo muhimu la kwanza lazima atafute mfumo wake. Kama atafanikiwa hili, atafanya vizuri', alisema.

2: Kikosi cha watoto chenye wakonge wa kuhesabu

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Kikosi cha Barca cha sasa kinaundwa zaidi na vijana, ingawa wapo wachache wakongwe wanaoendelea kuipigania, ingawa viwango vyao vimekuwa vikizua maswali.

'akija atakutana na manahodha wanne, Sergio Busquets, Sergi Roberto, Jordi Alba na Gerard Pique, pamoja na Marc-Andre ter Stegen, ambao alicheza nao,, atakutana na ugumu wa kuinua viwango vyao. Haitakuwa kazi nyepesi', alisema.

Kwa sasa Barcelona iko katika nafasi ya 9 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na alama 16 baada ya kucheza michezo 11, ikishinda 4, sare 4 na kupoteza 3. Hili sio jambo lililozoeleka kwa timu hiyo ambayo kushinda ni jambo la lazima kwao. Malalamiko ya kocha aliyetimuliwa, Koeman ni timu hiyo kujaa watoto, watoto ambao Xavi anakwenda kukutana nao.

Mbali na mashaka ya uwezo wake na uzoefu kwenye kufundisha, uzoefu wa Koeman umegonga mwamba, Xavi atatumia muarobaini gani kupata matokeo haraka?

3: Xavi ataziwesha presha za Barca na rais wake?

Kuwa Kocha wa Barcelona maana yake uwe kocha wa makombe, vinginevyo hautaonekana wa maana hata kama unafanya mambo ya maaana. Hakuna asiyemfahamu rais wa Klabu ya Barcelona anavyopenda mafanikio, lakini ni mmoja wa watu ambao, hawathamini na kumsujudia mtu hata akiwa na uwezo gani na umaarufu wa aina gani. Ana namna yake ya kufanya kazi inayoheshimika na pengine inaipa mafanikio timu hiyo.

Luis Suarez anaweza kuwa shuhuda wa namna alivyo Laporta. Kupitia Koeman, Suarez alipigiwa simu isiyozidi dakika moja kuondolewa klabuni hapo, licha ya kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa, wazoefu na walioisaidia timu hiyo katika misimu kadhaa aliyokuwepo akitengeneza safu ya ushambuliaji kali iliyofahamika kama MSN, akiwa pamoja na Neymar na Messi waliopo PSG kwa sasa.

aa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Barcelona, Joan Laporta

Messi wenyewe amelalamika juzi namna alivyotendewa katika siku zake za mwisho za Barcelona kabla ya kuhamia PSG. Mpaka Messi! Je Xavi atapona?

Ronald Koeman aliyetimuliwa wiki iliyopita na Laporta, alikua mfalme katika timu hiyo, baada ya kufunga goli muhimu katika muda wa nyongeza katika fainali ya kombe la Ulaya katika dimba la Wembley dhidi ya Sampdoria mwaka . Kwa Laporta alipata muda wa kiasi licha ya Barca kufanya vibaya msimu huu.

Pep Guardiola, kocha wa zamani wa Barcelona pengine alipata bahati ya kuongoza kikosi bora katika wakati wake, lakini tangu alivyopandisha kutoka Barcelona B, miaka 13 iliyopita, mawasiliano yake na mabosi hao wa zamani hayakuwa yakupigiwa shangwe, licha ya mafanikio aliyoipa Barcelona na hilo linaongeza presha kwa Xavi.

Kitakachomuokoa pengine kidogo ni kwa timu hiyo itakapokuwa inatwaa mataji mara kwa mara hasa la 'La liga' na la ligi ya mabingwa Ulaya, vinginevyo atakabiliwa na shinikizo kubwa.

' Pengine akija na watu kadhaa kwenye bechi la ufundi watamsaidia kufukia mambo mengi kuliko kusima peke yake', alisema Balague

4: Mafanikio kama mchezaji yatabeba matarajio yake kama kocha?

c

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Xavi ameisaidia Barca kupata makombe 25 katika miaka 17 aliyoichezea klabu hiyo.

Mhispania huyo ameichezea Barcelona kwa mafanikio makubwa katika kizazi ambacho pengine hakitaweza kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni kikivaa jezi ya Barcelona. Ukiacha Lionel Messi, Xavi amecheza katika vikosi vilivyokuwa na wakali wengi pale Barcelona akiwemo Andres Iniesta, Carles Puyol, Samuel E'too, Ronaldinho Gaucho, Samuel Eto'o na Thierry Henry.

Xavi ameichezea Barcelona michezo 779 na kushinda makombe 25 kati ya mwaka 1998 na 2015 kabla ya kutumia miaka yake ya mwisho ya soka akiwa na Klabu ya Al Sadd.

Ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Klabu hiyo kufanikiwa kubeba mataji mengi, lakini mafanikio yake kwa klabu hiyo akiwa kama mchezaji yanaweza kuyarejesha akiwa na kofia ya ukocha? tusubiri