Mabadiliko ya tabia nchi: Kwa nini watu wenye ulemavu ni waathirika wa majanga ya hali ya hewa?

Chanzo cha picha, ALBERTO PEZZALI
Waziri wa Israel Karine Elharrar aligonga vichwa vya habari duniani kote wiki hii baada ya kubainika kuwa hangeweza kuhudhuria mkutano wa kilele wa COP26 siku ya Jumatatu kwa sababu hakukuwa na miundombinu ya kumfanya ahudhurie kwa kutumia kiti chake cha magurudumu.
Kwa walemavu wengi, ilikuwa kama mfano wa mambo yalivyo na jinsi wanavyohisi kupuuzwa au kuwekwa nje ya mazungumzo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.
Hata hivyo walemavu ni miongoni mwa wale "walioathirika zaidi katika hali ya dharura", kwa mujibu wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa. Na dharura hizo - kutoka kwa moto wa porini hadi mafuriko - zinaweza kuwa za mara kwa mara kwa sababu ya shida ya hali ya hewa.
Kwa nini watu wenye ulemavu wanaathiriwa sana na mabadiliko ya hali ya hewa na tunaweza kufanya nini kuhusu hilo?
Kiharusi na upungufu wa maji mwilini kutokana na joto
Mnamo Julai 2018, wimbi la joto lilipiga Montreal, Canada. Hali ya joto lilipanda hadi kufikia nyuzi joto 35.5C kwa siku. Hospitali zilipokea na kuwahudumia wale waliopata athari za joto lililosababisha vifo vya watu 61. Robo ya wale walikuwa na schizophrenia.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Hiyo ni mara 500 ya idadi ya watu," anasema Prof Sébastien Jodoin, mtaalamu wa mabadiliko ya hali ya hewa kutoka Chuo Kikuu cha McGill, ambaye ana ugonjwa wa kuwa na sclerosis nyingi na anachunguza uhusiano kati ya haki za binadamu, ulemavu na mgogoro wa hali ya hewa.
Watu wengi walio na 'schizophrenia' hutumia dawa za kuzuia akili kutibu dalili zao. Inaweza kuwafanya wagonjwa wasistahimili joto, na kuongeza hatari ya kupata kiharusi cha joto na upungufu mkubwa wa maji mwilini, ambao unaweza kusababisha kifo.
Mafuriko
Msimu huu wa kiangazi, wakaazi 12 wanaoishi kwenye makazi maalumu ya walemavu katika mji wa Sinzig, nchini Ujerumani, walikufa kutokana na mafuriko yaliyotokea ghafla - hawakuweza kuhama. Mafuriko hayo yamehusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na wanasayansi na wanasiasa.
Dk Charles Williams, mwanasayansi wa hali ya hewa na mtafiti mwenzake katika Chuo Kikuu cha Bristol, ana tatizo la uti wa mgongo (SMA). "Kama mtumiaji wa kiti cha magurudumu, nisingeweza kuingia kwenye boti la mpira ili kuhamishwa," anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Visa kama hivyo viliibuka baada ya Kimbunga Katrina kupiga New Orleans mwaka wa 2005, na kusababisha mafuriko makubwa. Ripoti ya Baraza la Kitaifa la Walemavu lenye makao yake makuu nchini Marekani, iligundua kuwa walemavu wengi walitatizika kupata usaidizi.
Mabasi mengi ya uokoaji hayakuwa na lifti za viti vya magurudumu, makazi mengi ya dharura hayakuweza kufikiwa na watu wenye ulemavu huku walemavu wa kuona na wa kusikia hawakuweza kupata habari za usalama za ndani.
Maafa yanayohusiana na hali ya hewa, kama vile Kimbunga Katrina, yameongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Kwa hivyo ni nini kinahitaji kutokea ili kusaidia watu wenye ulemavu bora?
Andy Greene, kutoka kwa taasisi ya watu wenye ulemavu ya (DPAC), anaamini walemavu wanahitaji kuhusishwa zaidi katika mijadala ya mabadiliko ya hali ya hewa - haswa wakati sheria mpya zinatengenezwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nini kinachofuatwa?
Katika mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa wa COP26, baadhi ya masuala ya watu ulemavu na mabadiliko ya hali ya hewa yataguswa. Moja wapo ni miundo jumuishi ya miji inayostahimili hali ya hewa, wakati nyingine itaangazia athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya ya watu wenye ulemavu.
Prof Jodoin anasema mara nyingi serikali hazifikirii kuhusu "mahitaji mahususi ya watu wenye ulemavu". Lakini anaona COP26 kama "fursa ya kusukuma haki za walemavu".
Dk Williams anasema "kuna sababu za kuwa na matumaini" kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Anasema tatizo hadi sasa limekuwa ni "kukosekana kwa motisha na utashi" wa kufanya mabadiliko katika ngazi ya mtu binafsi na kisiasa.
"Ni wakati tu ndio utakaoonyesha kama mitazamo hii itabadilika. Kumekuwa na mabadiliko makubwa katika miaka 10 iliyopita, lakini hii inahitaji kuendelea."















