Mzozo Ukraine-Russia: Msanii mkongwe mwenye umri wa miaka 76 anayepambana na Putin

Eland brightened and cropped
Iliyochapishwa

Katika nyumba yake ndogo kwenye makazi ya St Petersburg, msanii mkongwe Elena Osipova mwenye umri wa miaka 76 ananionesha mabango ya kupinga vita ambayo ametengeneza.

Kwenye moja ameandika: "Putin ni vita. Hatutaki kufa kwa ajili ya Putin."

Mwingine anaonesha rais wa Urusi kuwa shetani, mwenye pembe za kishetani.

Elena ananiambia kwamba baada ya Urusi kushambulia Ukraine, alishtuka sana, hakula kwa siku tatu. Kisha, akiwa amejawa na hasira, alienda mitaani kuandamana.

Umati mdogo ulikuwa ukimpigia makofi: waliimba "Hakuna Vita!"

Lakini maafisa wawili wa polisi walimkamata na kumuondoa.

Law enforcement officers escort an elderly woman during an anti-war protest against Russia"s invasion of Ukraine, in Saint Petersburg, Russia

Chanzo cha picha, Reuters

Polisi bado hawajamrudishia mabango yake.

Ananieleza hivi: "Nilipewa maua nyekundu, maua mazuri. Lakini yalisinyaa haraka sana na kufa.

Walinikumbusha juu ya vijana waliouawa.

"Kwa hiyo nilitengeneza bango na kuandika kwamba watu walikuwa wakitumwa kuuawa.

Na kwenye bango jingine nilitoa wito kwa askari wa Urusi: 'Wekeni chini bunduki zenu na mtakuwa mashujaa.'

Katika mji mzima, kikundi cha haki za binadamu, Wamama wa Wanajeshi wa St Petersburg, wanaendesha simu ya dharura.

Wazazi hupiga simu, wakiwa na wasiwasi kuhusu watoto wao walioandikishwa kujiunga na jeshi, ambao baadhi yao tayari wanapigana nchini Ukraine.

Wengi wao huomba sana msaada wa kuwapeleka wavulana wao nyumbani. Kumekuwa na simu nyingi - lakini pia kuna shinikizo kubwa kutoka juu. Olga kutoka kundi hilo ananiambia inalazimishwa kufungwa.

"Mamlaka wanapendelea kuficha mambo, ili kuipa jamii picha potofu kuwa kila kitu kiko sawa jeshini. Wanawataka wamama wa askari kuwa na subira na kukaa kimya."

Lakini huko St Petersburg, na kote Urusi, mamlaka inajaribu kukusanya uungwaji mkono kwa kile ambacho jeshi la Urusi linafanya nchini Ukraine.

Elena brightened cropped
Maelezo ya picha, Nyumbani kwa Elena kumejaa kazi zake nyingi za sanaa ingawa si zote za vita

Idara ya waandishi wa habari ya Polisi ya St Petersburg imekuwa na shughuli nyingi.

Wametengeneza video kadhaa za ujanja, zikiambatana na sauti na nyimbo ili kuonesha kuunga mkono vikosi vya Urusi nchini Ukraine.

Katika moja, maafisa wa kutuliza ghasia huunganisha silaha na watu mitaani. Kamera inainama kudhihirisha kuwa umati umeunda herufi Z.

Alama hiyo imechorwa kwenye magari mengi ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine, na inatumika kuonesha kuunga mkono mashambulizi ya Urusi.

Na kuna Warusi wengi ambao wanaiunga mkono - ambao, kwa sasa, wanaamini kile ambacho vyombo vya habari vya serikali hapa vinawaambia: kwamba Urusi iko sahihi.

Nje ya Jumba la Makumbusho maarufu duniani la Hermitage, ninasimama ili kuzungumza na Nadezhda, ambaye yuko nje kwa matembezi.

Ananiambia: "Ninaipenda Nchi yangu na ninamwamini rais wangu, na ikiwa unafikiri Magharibi inaweza kututisha kwa kutunyima bidhaa, umekosea. Warusi hawaogopi baridi au njaa."

Lakini akiwa ndani ya nyumba yake, msanii Elena Osipova anasema hatakubali kamwe kuwa inachofanya Urusi nchini Ukraine ni sawa.

Mengi zaidi

"Kinachotokea ni fedheha. Watu wengi wanauawa. Mamlaka inajaribu kuamsha hisia za uzalendo kwa umma. Lakini yote ni udanganyifu. Na wengi wanadanganywa na propaganda ambazo zimeendelea kwa miaka mingi na zimebadilisha watu. . Ni mbaya sana."

Katika miaka ya hivi karibuni, Warusi wamejua vita vingi.

Vita vya Soviet huko Afghanistan, vita viwili huko Chechnya, jeshi la Urusi likihusika katika vita huko Syria.

Na sasa Ukraine. Ikulu ya Kremlin inasisitiza kuwa wanajeshi wake huko wanaendesha operesheni maalum ya kijeshi.

Lakini wengi duniani wanaiita vita vya Urusi.

line