Chelsea vs Liverpool: Matukio ya kukumbukwa ya fainali za michuano ya FA CUP

Chanzo cha picha, Getty Images
Chelsea na Liverpool leo zinacheza fainali ya 141 ya Kombe la FA katika uwanja wa Wembley. Liverpool, ambao waliwabwaga Chelsea katika fainali ya Kombe la Carabao mwezi Februari, wanaweza kuwa na msimu mzuri baada ya kutinga pia fainali ya Ligi ya Mabingwa, huku wakiwa nyuma kwa alama tatu nyuma ya Manchester City katika Ligi ya England zikisalia mechi mbili ligi kumalizika.
Mabingwa mara nane wa Kombe la FA, Chelsea wanaingia kwenye fainali kwa msimu wa tatu mfululizo - na wa tano katika misimu sita - baada ya kumaliza washindi wa pili wakibwagwa na Arsenal mnamo 2020 chini ya Frank Lampard na Leicester City mnamo 2021 chini ya Thomas Tuchel.
"Litakuwa pambano lingine gumu, kutokana na ubora na mwenendo wa Liverpool," alisema Tuchel. "Lakini hii ndiyo maana ya fainali ya kombe."
Liverpool watakuwa wanacheza fainali yao ya kwanza tangu 2012, walipofungwa 2-1 na Chelsea.Chelsea wameshinda taji hilo mara tano tangu Reds waliponyakua Kombe la FA mnamo 2006.
"Washabiki wa Liverpool hufanya matukio kama haya kuwa yao," bosi wa Reds Jurgen Klopp alisema. "Napenda hilo sana."
Ni fainali ya kwanza ya Kombe la FA kuchezwa mbele ya mashabiki wengi katika uwanja wa Wembley tangu Manchester City ilipoichapa Watford 6-0 mwaka 2019 iliyotazamwa na mashabiki 85,854. Sababu kubwa ni mlipuko wa janga la Corona.Pamoja na hamu ya wengi kwenye fainali ya leo ya FA CUP, yapo matukio kadhaa ya kukumbukwa yaliyowahi kutokea kwenye fainali za michuano hiyo mikongwe England.
Wachezaji wa Liverpool 'Kurap' katika fainali ya 1988

Hakuna anayelisahau tukio la fainali ya FA CUP ya mwaka 1988. Wimbo wa kufokafoka 'rap' ulioimbwa na wachezaji wa Liverpool wakiingia uwanjani kabla ya kuanza kwa mchezo huo. Wakivaa kama wanamuziki wa hiphop, makofia makubwa, miwani na cheni kubwa kubwa za dhahabu, walionekana kituko, lakini walitaka kuonyesha upande mwingine wa vipaji vyao vya kurap. Waliokuwepo ,iaka hiyo, ambayo Liverpool ilikuwa inatawala soka la Ulaya, lilikuwa tukio kubwa la kukumbukwa. Lakini katika mchezo huo wa Fainali ya FA CUP dhidi ya Wimbledon , iliyopigwa Mei 14, 1988, Liverpool ililala kwa bao 1-0, licha ya burudani yao ya .kurap' wimbo wa kuhusu klabu yao.
' Nitakuwa kofia kama patafungwa goli kwa muda uliosalia'

Kwa sasa soka kuonyeshwa kwewe runinga ni jambo la kawaida. Lakini mechi ya kwanza ya FA CUP kuonyeshwa katika Televisheni ilikuwa mwaka 1938 Preston ilipoilaza Huddersfield 1-0. Preston ilikuwa na nyota Bill Shankly, ambaye baadaye alioongoza Liverpool kutwa mataji mawili mfululizo akiwa meneja , mwaka 1965 na 1974.
Nini cha kukumbukwa? ilikua sare tasa mpaka dakika tisini na mbili za nyongeza, ikiwa mechi inaelekea kwenye marejeano, mtangazaji wa BBC Thomas Woodrooffe alisema: "Nitakula kofia kama patapatikana goli kabla ya kipyenga cha mwisho." Dakika moja baadaye George Mutch anafunga kwa mkwaju wa penati kuipata taji la FA Cup Preston. Woodrooffe baadaye alitekeleza ahadi yake, alikula kofia, ingawa ilikuwa kofia iliyotengenezwa kwa keki, na sio kofia ya kawaida.
Goli la ushindi la Ramsey, Arsenal ikitoka nyuma na kuizaba Hull

Chanzo cha picha, Laurence Griffiths
Kwa mara ya kwanza, katika historia ya Klabu, Hull City ilitinga fainali ya FA Cup, ingawa ilionekana kibonde, ilianza mchezo kwa kushangaza, kwa kuongoza kwa mabao 2-0 ndani ya dakika 8. Cha kukumbukwa katika mchezo huu, ni namna Arsenal ilivyoipambana na kurejesha mabao hayo kupitia kwa Santi Cazorla na Laurent Koscielny yaliyoifanya mechi hiyo kwenda dakika 30 za nyongeza kabla ya Aaron Ramsey kufunga bao la ushindi katika dakika ya 109. Bao lililohitimisha miaka 9 ya ukame wa makombe kwa kikosi hicho cha Arsenal kilichokuwa chini ya Arsene Wenger - likiwa kombe la kwanza kati ya matatu waliyokuja kutwaa katika miaka minne iliyofuata.
Toure anaipa taji la kwanza kubwa Man City katika miaka 35

Chanzo cha picha, Getty Images
Fainali ya Kombe la FA 2011 haikuwa ya kawaida, lakini hakuna shabiki wa Manchester City atakayejali hilo. Hakukuwa na bao hadi dakika ya 74 Yaya Toure alipoukwamisha mpira wavuni na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa City.
Kwa nini inakumbukwa? Kwa sasa Manchester City kushinda kitu inaonekana kuwa ni jambo la kawaida sana siku hizi, lakini haikuwa hivyo wakati huo na hili lilikuwa taji lao la kwanza kubwa baada ya kusubiri kwa miaka 35. Baada ya hapo mambo yakawa mazuri kwao, mataji matano ya Ligi Kuu ya Uingereza, Kombe jingine la FA na Kombe la Ligi sita yakafuata.












